Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres ameisifu Serikali ya Tanzania kwa jitihada zake za kutafuta amani nchini Burundi.

Guterres ametoa pongezi hizo wakati aliposimama kwa muda katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wa jijini Dar es Salaam akitokea Kenya.

Katibu Mkuu huyo mpya wa UN alisimama kwa ajili ya kufanya mazunguzmo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk Augustine Mahiga.

Pamoja na mambo mengine Guterres alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa serikali kwa juhudi zake za kutafuta amani nchini Burundi kupitia kwa Msuluhishi wa mgogoro huo, Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.

Aidha alisema anatambua mzigo mkubwa inaoupata kama nchi kutokana na kuendelea kupokea wakimbizi kutoka Burundi, na kuahidi UN kuendelea kuunga mkono jitihada za kutafuta suluhu ya kisiasa nchini humo.

Kwa upande wake Balozi Mahiga amewasilisha salamu maalum kutoka kwa Rais John Magufuli kuhusiana na hatua iliyofikiwa ya usuluhishi wa mgogoro wa Burundi na ushiriki wa Tanzania katika vikosi vya Umoja wa Mataifa vya ulinzi wa amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Balozi Mahiga pia amesema Tanzania imefurahishwa na ujio wake na Rais amempa mwaliko rasmi wa kufanya ziara nchini.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *