Kampuni ya uchimbaji almasi ya Petra Diamonds imesimamisha shughuli zake za uchimbaji katika mgodi wake uliopo Mwadui mkoani Shinyanga.

Hii imekuja siku chache tu baada ya kamati za bunge kuwasilisha ripoti zao kwa Rais John Pombe Magufuli kufuatia uchunguzi walioufanya katika sekta ya uchimbaji madini ya almasi na tanzanite.

Petra ambao ndio wachimbaji wakubwa wa almasi nchini Tanzania, wamekuwa wamejikuta kuwa kampuni nyingine ya kigeni kuingia katika mgogoro serikali ya Tanzania katika harakati za kufanya mageuzi katika sekta ya uchimbaji madini nchini humo.

Wiki mbili zilizopita, mamlaka nchini Tanzania ziliripoti kukamatwa kwa vifurushi vya almasi katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere ambavyo vilikuwa ni mali ya Petra na vilikuwa mbioni kusafirishwa kwenda Ubelgiji kuuzwa.

Maafisa wa serikali walisema Petra ilidanganya juu ya kiasi na thamani ya almasi hizo ambapo, wakati kampuni ya Petra ikisema almasi hiyo ilikuwa na thamani ya dola za kimarekani milioni 14.8, uchunguzi wa serikali ulibaini almasi hiyo ilikuwa na thamani ya dola milioni 29.5.

Hata hivyo, Petra imekanusha tuhuma hizo na kusema kwanza wao ni wawazi katika kuripoti thamani ya almasi yake lakini pia ni wakala wa serikali ndio unaokisia na kutoa thamani ya almasi inayochimbwa na kampuni hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *