Kampuni ya Star Media (T) Ltd, imetangaza rasmi kurusha matangazo ya Kombe la Dunia Urusi 2018 mbashara kupitia king’amuzi chake cha StarTimes na kuwawezesha wateja wake kufuatilia mechi zote 64 zitakazochezwa nchini humo kuanzia Juni mwaka huu.

Meneja Masoko wa kampuni hiyo, David Malisa alisema mwaka huu katika kombe la dunia la 21, StarTimes ni mrushaji rasmi wa michuano hiyo ambayo itaanza Juni 14 hadi Julai 15 nchini Urusi na matangazo hayo yatarushwa kwa lugha ya Kiswahili.

“Tumeamua kurusha matangazo hayo kwa lugha ya Kiswahili na hii ni katika jitihada zetu za kuienzi na kuikuza lugha yetu ya Kiswahili ambayo ni maarufu zaidi katika ukanda huu wa Afrika Mashariki,” alisema.

Aidha alisema matangazo hayo ya Kombe la dunia yataambatana na uchambuzi utakaofanywa na wachambuzi mahiri wa michezo nchini.

“Sambamba na kuzindua Kombe la dunia, StarTimes pia tunatangaza ofa kwa wapenzi wa soka, ambapo wateja watakaonunua king’amuzi au runinga zetu za kidigitali kuanzia Mei 2 hadi Juni 30 watapatiwa kifurushi cha juu hadi Julai 31 bure,” alisema.

Pia alisema wateja wao pia wanaweza kutumia simu za mkononi kupitia StarTimes kufuatilia michuano hiyo moja kwa moja.

Kwa upande wake, balozi wa Kombe la Dunia StarTimes, Wema Sepetu aliishukuru kampuni hiyo kwa kumteua na kusema kwa kushirikiana na mashabiki wake pamoja na wasanii wenzake kuhamasisha Watanzania kufuatilia matangazo hayo kupitia StarTimes.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *