Kampuni ya Acacia imesema ripoti kuhusu mchanga wa dhahabu aliyopewa Rais John Magufuli imejaa upotoshaji wa hali ya juu.

Kampuni hiyo ya uchimbaji madini nchini imependekeza kufanyika kwa uchunguzi mpya ambao ni huru ili kuweza kupata ukweli.

Kampuni ya  Acacia, yenye makao makuu jijini London  nchini Uingereza imesema kwamba imejaribu mara kadhaa kuomba nakala ya ripoti hiyo nzima pamoja na utaratibu wa kuchukua sampuli kwenye uchunguzi huo akini mpaka sasa haijapewa.

Acacia imekuwa ikilipa mrahaba ambao ni asilimia 4 kwa mujibu wa makubaliano kati yake na Serikali pamoja na sheria za Tanzania na kuongeza kuwa, pamoja na kuwa kweli kuna baadhi ya aina nyingine za madini kama chuma, sulphur, rhodium na mengineyo kwenye mchanga, aina hizo hazina thamani kibiashara na kampuni hiyo haipati mapato yoyote kutokana nayo.

Kampuni hiyo imesisitiza kuwa, imekuwa ikilipa mrahaba kwa mujibu wa sheria kwa madini wanayoyazalisha na kusema kuwa, katazo hilo la kusafirisha mchanga kutoka migodi hiyo miwili inaifanya kampuni hiyo kupoteza zaidi ya shilingi bilioni 2.2 kila siku, huku ikisisitiza itachukua hatua zote kuhakikisha haiendelei kupata hasara.

Taarifa hiyo ya jana imekuja zikiwa zimepita siku mbili baada ya kampuni hiyo kutoa taarifa nyingine ya kukosoa ripoti ya uchunguzi wa makinikia ambayo imewasilishwa kwa Rais.

Kupitia taarifa hiyo, Acacia ilidai kuwa, haijaona nakala ya ripoti hiyo ambayo inaonyesha kuwa kiwango cha madini kilichopo kwenye makinikia yanayoshikiliwa katika Bandari ya Dar es Salaam ni mara kumi zaidi ya kiwango kilichoainishwa kwenye data zilizowasilishwa awali.

Kwa msingi huo, uongozi wa Acacia ulisema kuwa unaendelea kusubiri nakala zaidi za ripoti hiyo kwa ajili ya kutolea ufafanuzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *