Kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia imethibitisha kuwa ipo katika mpango wa kupunguza wafanyakazi wake hasa walinzi wa mgodi huo.

Meneja habari na mahusiano ya jamii wa Acacia, Bi. Nectar Foya amesema kuwa kampuni hiyo itaingia mkataba na kampuni binafsi itakayoendesha shughuli za ulinzi wa migodi yake yote mitatu ya North Mara, Bulyanhulu na Buzwagi.

Kampuni hiyo imejikuta kwenye msukosuko mkubwa baada Rais John Magufuli kupiga marufuku kusafirisha makontena ya mchanga wa madini kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kuchenjua na kuunda kamati ya kuchunguza kiasi cha madini kilichokuwa ndani ya mchanga huo na kujua tathmini ya athari yake kiuchumi.

Kampuni hiyo imetangaza mara kadhaa kuwa zuio hili limewasababishia hasara kubwa ndani ya kampuni hiyo.

Walisema kuwa wanapata hasara ya dola za Marekani milioni moja (Tsh. bilioni 2.238) kila siku kutokana na katazo hilo la ghafla kutoka kwa serikali.

Kauli hii ameitoa baada ya tamko alilotoa Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodini Tanzania, Bw. Nicodemus Kajungu mwisho wa wiki iliyopita kwamba kampuni hiyo ipo kwenye mpango wa kupunguza wafanyakazi 400.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *