Serikali ya Uganda imekiondoa kwenye maktaba za shule za nchi hiyo kitabu ‘LOVE LESSONS’ kilichoandikwa na mwandishi maarufu wa vitabu vya watoto wa Uingereza Jacqueline Wilson.

Waziri wa maadili wa Uganda, Simon Lokodo amesema kuwa kitabu hicho kina maudhui ya mapenzi na ngono na hakifai kwa wanafunzi wa shule za msingi.

Kitabu hicho kinachoelezea kwa kiasi fulani kuhusu mwanafunzi wa kike wa miaka 14 aliyetokea kumpenda kimapenzi mwalimu wake wa kiume.

Waziri, Lokodo ameliambia gazeti la New Vision kuwa alitembelea shule ya Greenhill Academy na kukuta shule hiyo ina nakala za kitabu hicho na akaamrisha ziondolewe kwenye maktaba ya shule hiyo mara moja.

Gazeti la New Vision pia limeripoti kuwa wazazi wengi wa watoto wanaosoma nchini humo wamekasirishwa na uwepo wa kitabu hicho kwenye maktaba za shule hizo.

 Waziri Lokodo amejipatia sifa kwenye siku za karibuni baada ya kusimamia maadili ya nchi hiyo ambapo wiki iliyopita alipiga marufuku ufanyikaji wa sherehe za mashoga huku akiahidi kuingiza mashine za kutambua vifaa vya kielektroniki vinavyochukua picha na video za ngono mtandaoni.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *