Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inaanza vikao vyake leo ikiwa ni mwanzo wa safari ya saa 72 ya mabadiliko makubwa ya kiuongozi ndani ya chama hicho.

Vikao hivyo vinavyofanyika leo na kesho na kufuatiwa na Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ambao utafanyika kesho, vinatarajiwa kuleta sura mpya za wajumbe wa Kamati Kuu (CC) ambayo huzaa sekretarieti ya chama hicho chini ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli.

Tayari joto la mabadiliko limetawala hisia za makada wa CCM, huku majina ya wanasiasa wakubwa yakitajwa kutoka na mapya kuingia ndani ya CC.

Hisia za mabadiliko hayo zinachochewa na uamuzi wa hivi karibuni wa Rais Magufuli kuwateua watu wenye nafasi nyeti za uongozi ndani ya chama hicho kushika nafasi mbalimbali za kiserikali.

Uamuzi wake wa kuwateua Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Rajabu Luhwavi, Dk. Emmanuel Nchimbi, Dk. Pindi Chana na kabla ya hapo Dk. Asha Rose Migiro ambao wote ni wajumbe wa CC kuwa mabalozi, inatajwa kuwa msingi na chachu ya kutokea kwa mabadiliko.

Aidha, hatua ya kumteua Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, kunatajwa pia kuwa mwelekeo wa kuingia kwa sura mpya katika nafasi nyingine kadhaa ndani ya vikao vya sekretarieti na CC ya chama hicho.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *