Jeshi la Polisi nchini limesema inachunguza tuhuma zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda dhidi ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi Suzan Kaganda kuhongwa ili wasidhibiti matumizi ya shisha.

Makonda ametoa tuhuma hizo baada ya kudai kuwa viongozi hao wa polisi wamekuwa wakilegalega kusimamia ipasavyo kukomesha matumizi ya dawa za kulevya, aina ya shisha.

Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai katika makao makuu ya jeshi hilo, Kamishna wa Polisi, Robert Boaz amesema hayo jana wakati akijibu swali kuhusu hatua za jeshi hilo zilizochukuliwa kutokana na tuhuma zilizotolewa na Makonda.

Wiki hii wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Umeme katika Jiji la Dar es Salaam uliofanywa na Waziri Mkuu, Makonda aliwatuhumu viongozi hao wa polisi kwa kulegalega kusimamia suala hilo huku akihofia wanaweza kuwa wamehongwa na watu waliotaka kumhonga yeye lakini akakataa.

Makonda amedai watu hao walipanga mikakati ya kumshawishi kupokea Sh milioni tano kwa kila mmoja kwa mwezi yaani Sh milioni 50 ili asipige kelele kuhusu shisha na wao waendelee kupata faida.

Katika suala hilo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema atamwajibisha Makonda ikiwa hatatekeleza agizo hilo la kuondoa matumizi ya shisha katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Akijibu tuhuma hizo katika moja ya luninga nchini, Kamanda Sirro amesema mapambano dhidi ya watumiaji wa dawa hizo za kulevya za shisha yanaendelea na wameshakamata watuhumiwa wengi na kuongeza kuwa sasa kesi za wahusika wa biashara hizo ziko kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) mwenye mamlaka ya kuwafikisha mahakamani.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *