Kaburi la baba mzazi wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, Yustine Ndugai limefukuliwa na mabaki yake kuchukuliwa na ndugu zake ili kwenda kuzikwa upya katika Kijiji cha Ibagwe, wilayani Kongwa mkoani Dodoma.

Mabaki ya mzee huyo aliyefariki dunia Mei 22, 1992 yalichukuliwa na wanaukoo juzi wakiongozwa na Spika Ndugai.

Mwenyekiti wa umoja wa wazee kitongoji cha Katente Namba Moja, Joseph Kitafuma alisema walimpokea mzee huyo kijijini hapo kama mchimbaji mdogo wa dhahabu mwaka 1986.

Kitafuma alimuomba Spika Ndugai kuwajengea zahanati kwani aliyotibiwa baba yake wakati anaugua imechakaa sana na kusema zahanati hiyo itapewa jina la Ndugai, ombi ambalo kiongozi huyo wa bunge alilikubali.

Mbunge wa Bukombe, Dotto Biteko aliwataka wananchi kuona umuhimu wa kuwatunza wazazi na kuhamisha makaburi yao kwa kufuata mila na desturi za eneo husika.

Alisema kuwa, kitendo kilichofanywa na spika ni cha kuigwa kwani kinaonyesha anatambua umuhimu wa wazazi si tu wakiwa hai lakini pia baada ya kufariki dunia.

Miaka 25 tangu Yustine Ndugai ambaye ni baba mzazi wa Spika wa Bunge, Job Ndugai azikwe katika Kitongoji cha Katente mkoani Geita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *