Rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, Joseph Kabila amewasili nchini Tanzania kwa ziara ya siku tatu.

Amepokelewa na viongozi mbalimbali wa nchi akiwemo rais John Magufuli, makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan na Waziri wa mambo ya nje balozi Augustine Mahiga.

Katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Rais Joseph Kabila amepokea heshima ya kupigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa ajili yake na baadaye kushuhudia burudani ya vikundi vya ngoma.

Leo rais Joseph Kabila atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Rais John Pombe Magufuli, ataweka jiwe la msingi la jengo la mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na baadaye kushiriki dhifa ya kitaifa itakayofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Katika ziara yake Rais Kabila anatarajia pia kuzungumzia masuala ya kisiasa nchini mwake ambapo uchaguzi uliopangwa kufanyika Novemba mwaka huu umesogezwa mbele mpaka mwakani jambo ambalo limeleta sintofahamu kwa wananchi wa Congo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *