Jumla ya askari na maofisa 340 wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wamekabidhiwa bendera ya Tanzania tayari kwenda nchini Kenya kushiriki zoezi Imara 2016 ambalo litadumu kwa muda wa siku kumi na nne.

Mkuu wa Jeshi la Nchi Kavu, Meja Jenerali James Mwakibolwa, ndiye aliyewakabidhi bendera askari hao kwenye hafla iliyofanyika makao makuu ya Brigedi ya Mbuni iliyopo Monduli mkoani Arusha.

Mwakibolwa amesema askari hao wanaenda nchini Kenya kuungana na wenzao kutoka Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambazo ni Kenya, Rwanda ,Uganda na Burundi. Zoezi hilo litafanyika Mombasa nchini Kenya.

Amesema mazoezi hayo ni mwendelezo wa mazoezi ambayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka kwa kubadili nchi, ambapo mwaka jana ilikuwa ni mazoezi ya nadharia na mwaka huu ni mazoezi ya vitendo. Mwakibolwa, alisema lengo la mazoezi hayo ni kudumisha ushirikiano, kufahamiana na kujifunza ili kufanya kazi kwa juhudi na weledi.

Awali Mkuu wa Kikosi cha 303 Luteni Kanali, Longinas Nyingo amesema zoezi hilo linashirikisha askari 295 na maofisa 45 ambapo zoezi hilo litahusisha kukabiliana na ugaidi katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki .

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *