Jumla ya wawindaji haramu 570 wamekamatwa katika Hifadhi ya Serengeti kwa miezi sita mwaka jana kuanzia Julai hadi Desemba kutokana na opresheni ya kudhibiti majangili.

Takwimu hizo zimetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa, James Mbugi wakati akikabidhi mradi wa bwawa la maji katika vijiji vya Gibaso na Karagatonga vya Kata ya Kwihacha uliogharimu zaidi ya Sh milioni 74.

Mbugi amesema majangili hao wamefikishwa mahakamani na kufunguliwa mashitaka yanayowakabili.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kwihacha, Mstapha Masyani, alilipongeza shirika hilo kwa kuwachimbia bwawa na kuwapunguzia wafugaji kutembea mwendo mrefu kwenda kutafuta maji ya kunywesha mifugo yao.

 Masyani alitumia nafasi hiyo kulitaka shirika hilo kuongeza birika la kunyweshea mifugo ambapo amesema lililopo halitoshi kwa kuzingatia kuwa mifugo ndani ya kata hiyo ni mingi.

Vilevile ameomba wahisani hao kuwajengea birika la kunyweshea mbuzi na kondoo kwa sababu la kunyweshea ng’ombe halikidhi mahitaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *