Kamanda wa kanda maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro amesema kuwa jeshi la polisi Dar es Salaam limewakamata jumla ya watuhumiwa 13,626 na kuwafikisha mahakamani kwa makosa mbali mbali kwa mwaka 2016.

Sirro amesema kuwa matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha yamepungua kutoka 204 mwaka jana hadi 127 mwaka huu.

Idadi hiyo ni pungufu ya matukio 77, sawa na asilimia 37.7 huku matukio ya kutumia nguvu yamepungua kutoka 1,181 mwaka jana hadi 874 sawa na asilimia 26.

Kamishna Sirro alifafanua kuwa matukio ya mauaji, yamepungua kwa asilimia 11 ukilinganisha na mwaka jana, ambapo kulikuwa na jumla ya matukio 327 wakati kwa mwaka huu ni matukio 291 pungufu ya matukio 36.

Alisema matukio ya ubakaji, yameongezeka kutoka 972 mwaka jana hadi 1030 mwaka huu, sawa na asilimia sita wakati matukio ya ulawiti yameongezeka kutoka 310 mwaka jana hadi 383 mwaka huu sawa na asilimia 23.5.

Kwa mujibu wa Sirro, matukio ya uvunjaji yamepungua kwa asilimia 5.7 ambapo kwa mwaka jana kulikuwa na matukio 5,677 na mwaka huu matukio 5,355 sawa na upungufu wa matukio 322.

Kwa upande wa wizi wa magari, umepungua kwa asilimia 18.1 kutoka matukio 392 hadi 321 mwaka huu huku wizi wa pikipiki ukipungua kutoka pikipiki 2,644 mwaka jana hadi 2,191 ambapo matukio 453 yamepungua sawa na asilimia 17.1.

Wizi wa mifugo umepungua kutoka 197 mwaka jana hadi 163 mwaka huu sawa na asilimia 17.3 ikiwa ni pungufu ya matukio 34.

Akielezea watuhumiwa hao, Sirro alisema kuwa kati yao 52 walikutwa na silaha za kivita 67 na risasi 1,076, na watuhumiwa 126 walikutwa na dawa za kulevya aina ya mirungi kilo 75 na gramu 254.

Pia alisema kuwa watuhumiwa 7,625 walikutwa na bangi kilo 2,843 na gramu 78 huku watuhumiwa 269 walikutwa na cocaine kilo tatu na gramu 255 na heroine kilo moja na gramu 654.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *