Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ameitabiria ubingwa timu ya Simba baada ya kuanza kwa kasi na kuonesha kiwango cha hali ya juu katika mechi zake ilizocheza hadi sasa.

Julio amesema usajili uliofanywa na viongozi wa timu hiyo ndiyo ulioibadilisha timu hiyo na kuachana na mwenendo mbaya wa misimu minne nyuma na kuwataka mashabiki wa timu hiyo kuendelea kuipa sapoti ili wafurahie matunda yao ya uvumilivu.

Kocha huyo pia aliwataka wachezaji wa timu hiyo kuacha kubweteka na matokeo wanayoyapata hivi sasa badala yake kuendelea kupambana kuipigania timu ili waweze kufikia malengo waliyoyakusudia.

Simba, ndiyo timu pekee ambayo haijafungwa hata mchezo mmoja katika mechi tisa ilizocheza na kujikusanyia pointi 23 ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.

Mara ya mwisho Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, ilikuwa ni msimu wa mwaka 2011/12, tangu hapo timu hiyo ilipotea na kujikuta ikiwa na mwenendo mbaya huku mara tatu ikimaliza msimu katika nafasi za tatu na nne.

Leo Simba inatarajiwa kucheza na Mbao kwenye mechi ya ligi kuu Tanzania Bara katika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *