Nahodha wa klabu ya Azam, John Bocco amesema kuwa leo hatoshangilia kama akishinda goli kwenye mchezo wa kombe la Shirikisho dhidi ya Cosmopolitan kutokana na kutambua mchango wao wa kumtoa hadi kusajiliwa na Azam FC.

Bocco atakuwa akirejea kucheza dhidi ya timu yake hiyo ya zamani ambayo ndiyo imemtoa hadi kupata nafasi ya kusajiliwa na Azam FC miaka tisa iliyopita wakati ikishiriki ligi ya madaraja ya chini na kuipandisha rasmi Ligi Kuu mwaka 2008.

Akizungumzia mchezo huo Bocco amesema kuwa wao kama wachezaji wana morali kubwa kwa ajili ya kucheza mchezo huo, huku akidai kuwa wamejipanga kupambana uwanjani kuhakikisha wanashinda mtanange huo.

Azam FC itakuwa na kibarua cha kuzifuata Simba na Yanga ambazo tayari zimetangulia hatua ya 16 bora katika mchezo wa raundi ya tano ya michuano ya Kombe la Shirikisho utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Mechi nyingine zinazopigwa leo ni Stand United ambayo itacheza na Polisi Mara kwenye Uwanja wa Karume Mara wakati Ndanda itacheza na Mlale JKT kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *