Jeshi la Polisi nchini limesema kuwa kuwa ndani ya Jeshi hilo hakuna ajira zilizotangazwa na kuwataka wananchi wote kuwa makini na mtandao wa matapeli.

Kauli hiyo imetolewa leo na msemaji wa jeshi hilo nchini, ACP Advera John Bulimba kufuati kuibuka kwa kikundi kidogo cha matapeli wanaozunguka katika maeneo mbalimbali hususani vijijini na kuwalaghai vijana kwamba watawapatia ajira ndani ya Jeshi la Polisi jambo ambalo siyo la kweli.

Amesema kuwa kikundi hicho cha matapeli kilichoibuka hivi karibuni kinazunguka maeneo mbali mbali na kuwadanganya vijana kuwa wao ni waajiriwa wa Jeshi la Polisi na kujipatia fedha kwa udanganyifu huo.

Amesema mfumo wa ajira ndani ya Jeshi la Polisi ni wa wazi na una utaratibu maalum ambao hutangazwa kwa wananchi kwa mujibu wa taratibu za Jeshi hilo.

Kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi limetoa onyo kali kwa wote wenye tabia hiyo ya utapeli kuacha mara moja na endapo mtu yeyote atabainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Mwisho Jeshi hilo limetoa rai kwa wananchi wote wenye taarifa za matapeli hao kuzifikisha haraka katika kituo chochote cha Polisi kilicho karibu ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *