Jeshi la polisi mkoni Kigoma limesema wanamsubiri Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe awasili mkoani hapo, ili kuweza kutoa taarifa rasmi ya kuteketea kwa nyumba yake iliyopo Mwandiga mkoani Kigoma.

Kamanda wa polisi mkoa wa Kigoma Ferdinand Mtui, amesema polisi inachelea kutoa ripoti hiyo kwa sababu mwenyewe mhusika (Zitto Kabwe) hayuko Kigoma, hivyo hawawezi kujua thamani ya mali ambazo zilikuwepo.

“Bado tunaendelea mpaka mwenyewe apatikane na yuko Dodoma, kwa sababu huwezi kujua gharama mpaka yeye mwenyewe awepo, na nyumba ambayo imeungua ni nyumba ndogo aliyokuwa anakaa mlinzi sio nyumba kubwa”, amesema Kamanda Mtui.

Kwa upande wake Zitto Kabwe amewataka wananchi kuwa na subira juu ya ripoti ya tukio hilo, huku akiwashukuru wananchi waliosaidia kuzima moto huo.

“Nawashukuru Jeshi la Zimamoto, majirani zangu pamoja na wananchi wenzangu kwa ushirikiano walioutoa mpaka kuuzima moto, kwa sasa Jeshi la Polisi wanafanyia kazi kujua chanzo cha ajali, naomba wananchi wawe watulivu wakati polisi wanaendelea na uchunguzi husika”, ameandika Zitto Kabwe.

Hapo jana moto uliteketeza nyumba ya Zitto Kabwe mkoani Kigoma ikiwa na  vitu ambavyo thamani yake bado haijawekwa wazi, lakini hakuna mtu aliyeathirika na ajali hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *