Jengo la Amani na Usalama lililopo Makao Makuu ya Umoja wa Afrika (AU) mjini Addis Ababa nchini Ethiopia limetangazwa rasmi kuwa litaitwa Mwalimu Julius Nyerere.

Jengo hilo limepewa jina hilo rasmi katika hafla ya chakula cha mchana, iliyofanyika jana na kuhudhuriwa na Rais John Magufuli pamoja na marais mbalimbali wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika.

Wengine waliohudhuria mkutano huo ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, mawaziri na mabalozi mbalimbali wanaohudhuria Mkutano wa 28 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika unaoendelea mjini humo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, akizungumza katika hafla hiyo, Rais Magufuli aliwashukuru viongozi wote wa AU kwa kuamua jengo hilo liitwe jina la Mwalimu Julius Nyerere ikiwa ni kutambua mchango wake katika kupigania amani na usalama na alibainisha kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa Mwafrika halisi na kiongozi mahiri na shupavu.

Dk Magufuli aliongeza kuwa Mwalimu Nyerere alitoa mchango mkubwa katika kupambana na ubaguzi na unyonyaji wa kila aina, alisaidia ukombozi wa nchi nyingi za Afrika, na hata alipong’atuka katika hatamu za uongozi wa Taifa la Tanzania aliendelea kutoa mchango wake kupigania amani katika nchi za Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *