Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo amepiga marufuku kwa wafanyabiashara wa Manispaa ya Dodoma kupanga bidhaa zao barabarani na kutakiwa kutumia masoko au maeneo rasmi.

Jafo ametoa kauli hiyo alipokuwa akikagua ujenzi wa barabara ya Sango iliyopo katika soko kuu la Majengo, pamoja na ujenzi wa dampo la kisasa.

Jafo amesema serikali imewekeza fedha nyingi kwenye barabara, lakini haionekani kutokana na watu kupanga bidhaa zao.

Amesema kupangwa kwa bidhaa za nyanya au vitunguu barabarani kumekuwa kukichafua barabara na wakati mwingine kusababisha zisipitike kwa urahisi.

Hata hivyo, alisema kwa kuwa vikao vimeanza vya kupendekeza Dodoma iwe Jiji, ni lazima iwe na thamani ya jiji kwa watu kutumia masoko na si kupanga bidhaa barabarani.

Kwa upande wake mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi, aliahidi kusimamia sheria ndogo za manispaa kuhakikisha wafanyabiashara wanafanya biashara zao kwenye maeneo yaliyopangwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *