Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Hapi ambaye ni kaimu mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam amekabidhi mifuko 100 ya saruji ambayo ni sawa na tani tano kwa Jeshi la Polisi.
Hapi alikabidhi mifuko hiyo jana baada ya kutembelea makazi ya polisi wanaoishi Kituo cha Polisi Msimbazi, ambapo zinaishi familia 72 na kukuta jengo hilo lenye ghorofa nne ni chakavu, limejengwa tangu enzi ya mkoloni.
Alisema ametoa msaada huo kwa kuwa jeshi la polisi linafanya kazi kubwa na nzuri usiku na mchana, kwa kulinda raia na mali zao, hivyo nalo linapaswa kuangaliwa kwa jicho la karibu.
Ameitaka jamii kuliangalia jeshi hilo ili kuhakikisha wanakaa katika mazingira mazuri ili nalo liendelee na kasi ya kuwalinda wananchi na mali zao.
Alitaka viongozi kusimamia mifuko hiyo, iliyotolewa ili ikafanye kazi iliyokusudiwa, endapo itapungua aliomba apewe taarifa ili aangalie njia ya kuongeza.