Gavana wa jimbo la Mombasa nchini Kenya, Hassan Joho anakabiliwa na tuhuma za kughushi cheti cha mtihani wa kidato cha nne nchini humo.

Baraza la Taifa la Mitihani Kenya (KNEC) linadai mwanasiasa huyo wa chama cha upinzani cha ODM alighushi cheti cha mtokeo ya mtihani wa kidato cha nne ili kumuwezesha kukubaliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi.

Joho ambaye ni naibu kiongozi wa chama cha ODM cha waziri mkuu wa zamani Raila Odinga, amekanusha madai hayo na kudai kwamba serikali imeibua tuhuma hizo ili kumpiga vita.

Barua ya kaimu afisa mkuu mtendaji wa baraza la mitihani Bi M G Karogo ambayo ilitumwa kwa maafisa wakuu wa uchunguzi wa jinai inaonesha mwanafunzi kwa jina Ali Hassan alifanya mtihani wake katika shule ya sekondari ya 1993 na akapata alama D- ambayo haiwezeshi mtu kujiunga na chuo kikuu.

Gavana huyo anadaiwa kughushi cheti cha kuonesha alipata alama ya C+ katika mtihani wa mwaka 1992 na akatumia cheti hicho kujiunga na chuo kikuu cha Nairobi ingawa hakumaliza masomo yake.

Joho alijiunga na Chuo Kikuu cha Kampala na akafuzu na shahada katika usimamizi wa biashara mwaka 2013.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *