Mahakama kuu kanda ya Dar es Salaam, imemtaka Gavana wa Benki Kuu (BoT), Benno Ndulu na Mwendeshaji wa benki ya FBME, Lawrence Mafuru wafike mahakamani kujieleza jinsi watakavyotekeleza amri iliyoitaka BoT kulipa Sh bilioni 92.

Maofisa hao wanatakiwa kuieleza mahakama watakavyoilipa kampuni ya Coast Textiles Ltd fedha hizo na kama watashindwa kufanya hivyo, watafungwa jela kama wafungwa wa kesi ya madai.

Utekelezaji wa amri hiyo unatokana na uamuzi wa shauri namba 129 la mwaka 2009, ulioiamuru benki ya FBME kuilipa kampuni ya Coast Textiles Ltd fedha hizo baada ya kukamata kiwanda chake na kukiuza kwa kampuni ya Five Star Investment ltd.

Uuzwaji wa kiwanda hicho ulitokana na mgogoro wa ulipaji mkopo ambao kampuni ya Coast iliuchukua katika benki hiyo.

BoT inahusishwa kwenye shauri hilo kutokana na kuchukua uendeshaji wa benki ya FBME baada ya benki hiyo kuhusishwa na utakatishaji fedha nchini Cyprus.

Maofisa hao walitakiwa kufika mahakamani hapo Septemba 16 mwaka huu kwa ajili ya kueleza jinsi watakavyotekeleza amri hiyo, lakini hawakufika kwa kuwa wamewasilisha maombi ya kusimamisha shauri hilo ambayo yamepangwa kusikilizwa leo mbele ya Jaji Ama Munisi.

Katika kesi ya msingi iliyofunguliwa na kampuni ya Coast, mahakama iliamuru FBME iilipe kampuni hiyo Sh bilioni 21.2 na riba ya asilimia 21 kwa mwaka tangu Juni 28, 2001 hadi hukumu ilipotolewa, Julai 27, 2015.

Baada ya uamuzi huo, walalamikaji walipeleka maombi ya utekelezwaji wa hukumu hiyo, ambayo ukijumlisha na riba ni sawa na Sh bilioni 92.2.

Kutokana na maombi hayo, mahakama ilimuelekeza Gavana wa BoT kukamata akaunti mbili zinazomilikiwa na benki ya FBME, hata hivyo BoT iliwasilisha maombi ya kuchunguzwa kwa umiliki halali wa akaunti zinazoshikiliwa na kuiomba mahakama isitishe amri hiyo kwa kuwa BoT siyo miongoni mwa walalamikiwa kwenye shauri la msingi.

BoT iliingilia kati suala hilo, kwa kuwa kwa sasa ndiyo inayosimamia uendeshwaji wa benki ya FBME kwa ajili ya kulinda amana za wateja baada ya benki hiyo kuhusishwa na utakatishaji fedha.

Baada ya kusikiliza maombi hayo, mahakama iliondoa amri hiyo na kuamuru benki hiyo ilipe fedha, hata hivyo walalamikaji waliwasilisha maombi mengine ya kukazia hukumu katika Mahakama Kuu.

Katika maombi hayo Msajili wa Mahakama Kuu, Projest Kahyoza alitoa siku saba kwa maofisa hao kufika mahakamani kujieleza jinsi watakavyolipa fedha hizo na wakishindwa watafungwa jela kama wafungwa wa madai.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *