Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) muda wowote kuanzia sasa litatuma maofisa wake kuja nchini kufuatilia tuhuma za utakatishaji fedha alizonazo Rais wa shirikisho la soka nchini TFF, Jamal Malinzi.

Malinzi na wenzake ambao ni Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa na Mkurugenzi wa Fedha wa shirikisho hilo, Nsiande Mwanga walipandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa makosa 28 yakiwemo ya utakatishaji fedha.

Baada ya kusomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbord Mashauri katika kesi yao namba 213, watuhumiwa hao walinyimwa dhamana na kupelekwa mahabusu hadi kesi yao itakaposikilizwa tena keshokutwa Jumatatu.

Makamu wa Rais wa TFF, Wallace Karia alisema Fifa tayari ina taarifa za viongozi hao wa TFF kukamatwa na kupandishwa kizimbani kisha kwenda mahabusu.

Ni wazi kwamba kuna ugumu wa Malinzi kuwahi usaili kwani leo ndiyo mwisho na yeye atafikishwa mahakamani keshokutwa Jumatatu.

Hata hivyo, jana mchana zilivumishwa habari za rais huyo kuwasilisha barua kwa kamati ya uchaguzi ya kuomba udhuru wa kutofanya usaili katika siku zilizopangwa ili afanyiwe Jumatatu ijayo.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *