Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani amesema Serikali imedhamiria kufufua na kuyawezesha mashirika yake yote kufanya biashara na kuzalisha faida ili kujitegemea na kuachana na utegemezi wa ruzuku toka Serikalini.

Akizungumza katika majumuisho ya ziara yake ya siku tatu mkoani Mbeya Eng. Ngonyani amezitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA), na Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) kubuni vyanzo vya mapato.

Amewataka TAA kuhakikisha ndege nyingi zinautumia uwanja wa ndege wa kimataifa Songwe kwani ukitumika vizuri unaweza kuwa kitovu cha uchumi kwa ukanda wa kusini na nchi jirani kutokana na ubora wake.

Naibu Waziri huyo amezungumzia umuhimu wa TAZARA kutafuta soko la ndani badala ya kutegemea soko la nje pekee kwani kufanya hivyo kutapunguza mizigo mingi inayosafirishwa kwa njia ya barabara na kuhamia kwenye reli hali itakayopunguza msongamano na uharibifu wa barabara.

Ameziagiza taasisi zilizo chini ya Wizara ya ujenzi kuiamini TEMESA, kufanya kazi na taasisi hiyo na kulipa madeni zinazodaiwa ili kuiwezesha kukua na kuaminika kwa taasisi nyingine na sekta binafsi.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *