Rais wa Ufilipino, Rodrigo Duterte amesema kuwa yupo tayari mwanawe auawe iwapo madai kwamba anahusika katika biashara ya madawa ya kulevya yatakuwa ya kweli.

Ameongeza kwamba polisi ambao wataendesha mauaji hayo watalindwa dhidi ya kufunguliwa mashitaka.

Paolo Duterte mwenye umri wa miaka 42, alifikishwa mbele ya jopo la maseneta alipokana madai yaliyotolewa na wabunge wa upande wa wapinzani kwamba alikuwa mwanachama wa kundi la Wachina lililosaidia kuingiza ndani ya nchi hiyo madawa ya kulevya aina ya ‘crystal methamphetamine’.

Rais Duterte hakumaanisha hasa madai hayo dhidi ya mwanaye, lakini alisisitiza maneno yake aliyoyasema wakati wa kampeni ya uchaguzi mwaka jana kwamba hakuna mwanaye yeyote anayejihusisha na madawa ya kulevya, lakini wangekabiliwa na adhabu ngumu zaidi iwapo wangefanya hivyo.

Duterte (72) alishinda uchaguzi wa rais kwa kampeni kali aliyoendesha akiahidi kuyatokomeza madawa katika jamii kwa kuua wauaji na watumiaji wa madawa hayo wapatao 100,000.

Tangu ashike madaraka katikati ya mwaka jana, polisi wameripoti kuua watu zaidi ya 3,800 katika oparesheni dhidi ya madawa ya kulevya wakati maelfu wameuawa katika mazingira yasiyoelezeka.

Maelfu ya wakosoaji na wafuasi wake, walifanya mikutano mbalimbali jana (Alhamisi) kujadili vita hiyo kali ya mauaji na vitisho vya kijeshi mitaani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *