Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dkt. Hussein Mwinyi amesema kuwa hakuna sheria yoyote inayowapa haki wanajeshi kuwatesa raia au kuvunja sheria kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mwinyi ametoa ufafanuzi wa mfumo huo wa jeshi wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Lucy Magereli (Chadema) aliyetaka kujua ni sheria zipi zinawapa askari haki ya kutesa raia.

Alisema matukio ya wanajeshi kushambulia raia au raia kushambulia wanajeshi, mara nyingi yamekuwa yakijitokeza wakati pande mbili zimetofautiana kauli, katika ulevi, wivu wa kimapenzi na hata ujambazi.

Dk Mwinyi amesema, katika kushughulikia hali hiyo, mara nyingi kesi hufunguliwa kwenye mahakama za kiraia na hukumu hutolewa kwa mujibu wa sheria zilizopo nchini.

Waziri Mwinyi amesema kuwa  “Hakuna mtu aliye juu ya sheria na inashauriwa kwamba watu wanaokumbwa na kadhia ya kushambuliwa na askari wapeleke mashtaka kwa mujibu wa taratibu zilizipo ili sheria ifute mkondo wake.”

Pia ameongeza kwa kusema kuwa “Kwa taratibu za Jeshi la Ulinzi, afisa au askari anapotiwa hatiani na mahakama za kiraia na kuhukumiwa adhabu ya kifungo au nyinginezo, hupoteza sifa za kuendelea kulitumikia JWTZ,”.

Mwinyi amemaliza kwa kusema kuwa maafisa na askari wa jeshi wamekuwa wakiaswa kuishi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizipo nchini.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *