Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein amesema jitihada za kuimarisha huduma za bandari zitafanikiwa endapo waliopewa dhamana ya kuzisimamia na kufanya kazi katika maeneo hayo wataacha kufanya kazi kwa mazoea.

Dk Shein aliyasema hayo katika hafla ya uzinduzi wa vifaa vipya vya kuhudumia mizigo bandarini iliyofanyika katika Bandari ya Malindi, mjini Unguja ikiwa ni sehemu ya sherehe za miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema, kwa kuwa bandari ni lango la biashara, ni lazima wafanyakazi wa Shirika la Bandari waendelee kubuni njia bora za kuongeza ubora wa huduma kwa wanaowahudumia na kujitangaza zaidi kukabiliana na ushindani uliopo.

Rais huyo amesema ili azma hiyo ifanikiwe, mambo ya kuzingatia ni pamoja na kuwa waaminifu, waadilifu, kuepuka urasimu katika kutoa huduma, kujiepusha na rushwa na kuhakikisha wateja wanahudumiwa kwa muda mfupi.

Dk Shein amesema ununuzi wa vifaa hivyo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 ambayo imeanza kutekelezwa kwa kasi kubwa katika sekta mbalimbali ikienda sambamba na uimarishaji wa bandari nchini.

Pia amesema katika kipindi cha pili cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, awamu ya saba, Serikali itaimarisha na kuendeleza bandari ya mkoani kwa kuipatia vifaa vya kisasa vya kuhudumia abiria na mizigo.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *