Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inawashikilia watu wawili kwa kukutwa wakisafirisha dhahabu yenye uzito wa kilogramu 6.2 iliyokadiriwa kuwa na thamani ya shilingi 500.3 milioni isivyo halali.

Mkurugenzi wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko aliwataja watu hao kuwa ni Akifa Mohamed na Jaffer Hussein na kueleza kwamba walikamatwa katika eneo ambalo hutumiwa na wasafiri wanaokwenda Zanzibar.

Mhandisi Kakoko alieleza kwamba tukio hilo lilitokea Oktoba 10, mwaka huu saa 5:20 usiku eneo la Azam Sea Link/DMI, wakati askari wa TPA na wa vyombo vya ulinzi na usalama, walipokuwa katika ukaguzi wa abiria, mizigo na magari yaliyokuwa yakiingia katika meli ya MV Azam Sea Link – I.

Alisema watu hao wawili walikuwa wa mwisho kufika eneo hilo wakiwa na gari aina ya Toyota Noah na begi lililokuwa na dhahabu hizo lilifichwa katika siti za nyuma.

Aliongeza kuwa mwanzoni watuhumiwa hao walikataa kupekuliwa ila baada ya kubanwa ndipo walikubali na mzigo huo kupatikana.

Kakoko alisema watuhumiwa hao walipohojiwa mmoja alieleza kwamba nyaraka zote za madini hayo ziko Zanzibar lakini uchunguzi umebaini kuwa hakuna nyaraka zozote, huku mwingine akieleza alipewa dhahabu hizo azisafirishe.

Alileza kuwa watu hao wanashikiliwa katika kituo cha Polisi cha Bandari ya Dar es Salaam na watafunguliwa shtaka la kupatikana na madini isivyo halali.

Dereva wa gari hilo alikimbia baada ya kushtukiwa, na gari linashikiliwa huku dereva huyo akisakwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *