Mahakama Kuu kitengo cha Ardhi imeiondoa kampuni ya Quality Group Ltd inayomilikiwa na mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji kwenye jengo la Quality Plaza baada ya kushindwa kulipa deni la bilioni 13.

Jengo hilo la Quality Plaza linamilikiwa na Mfuko wa Pension wa PSPF ambao umetoa idhini kwa kampuni hiyo itolewe haraka ndani ya jengo hilo.

Kampuni ya Udalali ya Mahakama ya Yono waliopewa idhini na mfuko huo kuwatoa wadaiwa hao baada ya kushindwa kesi, kufuatia hukumu ya Mahakama Kuu iliyotolewa Novemba 24 mwaka huu, walitoa vyombo nje baada ya kupewa saa 24 kuondoa kwa hiari.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yono, Scholastika Kevela amesema kuwa walitoa notisi ya saa 24 waliyoibandika juzi kwenye ofisi hiyo wakiwataka waondoke wenyewe kabla ya amri hiyo halali ya Mahakama haijaisha ifikapo leo asubuhi.

Amesema Mfuko wa PSPF,unaidai Kampuni ya Quality Group fedha hizo za upangaji, lakini kila anapotakiwa kulipa amekuwa akigoma na kukimbilia mahakamani kuweka pingamizi la kulipa ili aendelee kukaa bure na kwamba uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa Novemba 24, umemtaka aondoke ndani ya saa 24 na kulipa deni analodaiwa.

Amesema pamoja na kutoa vitu vyake ndani ya jengo hilo amepewa muda wa siku 14 kisheria awe amelipa deni hilo na kama atashindwa kulipa mali zake zitakamatwa na kuuzwa ili kupata fedha za kulipa deni analodaiwa na PSPF.

Kampuni nyingine zilizoamriwa kuondoka ndani ya jengo hilo ni Gaming Management Ltd, Q-cosult Ltd, International Transit Investiment ltd.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *