Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema ameunda timu ya watu wanne itakayofuatilia malipo ya fidia ya ardhi kwa ajili ya wananchi walioondolewa katika eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.

Timu hiyo imeundwa juzi wakati wa mkutano wa Mkuu huyo wa Wilaya na wananchi hau huku akisema timu hiyo itahusika pia kufuatilia ulipwaji wa viwanja.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mjema amesema ataunda timu nyingine ya watu sita itakayochunguza tuhuma zilizotolewa na wakazi hao dhidi ya maofisa waliodaiwa kuwa si waaminifu, wanaodaiwa kujilimbikizia viwanja na kuwagawia wasiostahili.

Mjema aliamua kuunda timu ya kufuatilia malipo hayo ya fidia baada ya maelezo ya Mhandisi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), William Shechambo mkutanoni hapo kutowaridhisha wananchi, kutokana na kutoonesha lini watalipwa fidia na kupewa viwanja.

Awali, wananchi hao waliwasilisha malalamiko yao mbele ya Mjema na maofisa wengine waliokuwepo kwenye mkutano huo ambao walidai kuwa hawafahamu hatma ya maeneo yao yaliyochukuliwa na TAA kwa ajili ya utanuzi wa kiwanja.

Wananchi hao kutoka katika mitaa ya Kipunguni, Kigilagila na Pugu Kinyamwezi walidai kuwa hawajalipwa fidia kama walivyoahidiwa na Serikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *