Kampuni ya simu za mkononi Zantel imepewa siku saba kulipa kiasi cha Sh milioni 700 inazodaiwa na manispaa hiyo ikiwa ni kodi ya eneo kuanzia 2009 hadi 2014.
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya ya Kinondoni Ally Hapi wakati alipotembelea ofisi za kampuni hiyo, jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa wilaya huyo amesema Manispaa ya Kinondoni iliingia mkataba na Zantel mwaka 2009 kuwakodisha eneo ambalo walitakiwa kulipa kila mwezi, lakini mpaka sasa hakuna kiasi chochote kilicholipwa huku mkataba huo ukionesha umemalizika muda tangu mwaka 2014.
Aidha, alisema kwa kuwa mkataba huo ulikuwa unaishia Januari 31, 2014 na kwa sababu mwaka 2009 ni mbali na viwango vya thamani ya ardhi katika eneo hilo vilikuwa vinapanda hivyo amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Aron Kagurumjuli, kufanya ukokotozi kuangalia pale mkataba ulipoishia kuona kama thamani ya ardhi ndiyo ile iliyokuwa awali au ilipanda ili kampuni hiyo ilipe kulingana na ongezeko.
Mkuu huyo wa wilaya pia amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa hiyo na Zantel ifikapo Januari 31 mwaka 2017 wakae kuangalia mkataba na kuingia mkataba mpya utakaozingatia nafasi ya serikali kukusanya mapato kwa mujibu wa thamani ya ardhi iliyopo sasa, utakaoonesha wazi fedha zinalipwa wapi na lini na kiasi gani.