Jeshi la Polisi wilaya ya Kinondoni wamekabidhiwa orodha ya majina ya watu 21 wanaojihusisha na uvuvi haramu.

Orodha hiyo imetolewa na mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi na kumkabidhi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Suzan Kaganda.

Hapi alikabidhi orodha hiyo jana wakati akizindua kampeni maalumu ya mapambano dhidi ya wavuvi haramu sambamba na uchomaji zana zisizofaa zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 60.

Akizungumza katika shughuli ya uchomaji zana hizo katika ziara aliyoifanya jana katika Kata ya Mbweni, Hapi amesema katika orodha hiyo pia wamo viongozi wawili ambao hakutaja majina wala vyeo vyao.

Katika orodha hiyo, mkuu huyo wa wilaya amesema anafahamu vinara wa matukio hayo wana nguvu kubwa lakini Serikali imedhamiria kupambana na kutokomeza vitendo hivyo.

Amesema wavuvi haramu wamekuwa wakitumia milipuko ambayo ni hatari na kama haitazuiliwa, inaweza ikachangia kujitokeza kwa matukio ya kihalifu pamoja na ugaidi.

Amesema wameshuhudia matukio mbalimbali yanayojitokeza kwa sababu ya uvuvi haramu ikiwamo watumiaji wa zana hizo kukatika mikono na miguu, hivyo ipo haja ya kila mwananchi kuwafichua watu wanaojihusisha na uvuvi haramu.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *