Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema amelitaka Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) kufanya uchunguzi katika dampo la Viwege kata ya Majohe.

Amesema ikiwa NEMC itashindwa kuchukua hatua dhidi ya utitirishwaji wa maji yanayodaiwa kuwaathiri wakazi wa eneo hilo itabidi lifungwe kwa kuwa wasimamizi wa dampo hilo watakuwa wameshindwa kutunza mazingira.

Mjema alitoa agizo hilo alipotembelea eneo la dampo hilo na kusikiliza malalamiko ya wananchi kuhusu maji hayo wanayodai kuwa na sumu ambayo inawaathiri wakazi na watoto wadogo.

Alisema wasimamizi wa dampo hilo hawapaswi kutiririsha maji yanayotoka kwenye taka katika makazi ya watu, bali walipaswa kutengeneza miundombinu mizuri ya maji hayo ili kuepusha athari za magonjwa kwa wananchi.

Akizungumzia athari za maji hayo, Mwanaisha Rajabu ambaye ni mkazi wa eneo hilo alisema, maji hayo yamekuwa yakiwasababishia magonjwa ikiwemo watoto kupata upele kutokana na maji hayo.

Aliomba serikali kuangalia uwezekano wa kulifungia dampo hilo kwa muda hadi litakapofanyiwa marekebisho ya kutotiririsha maji hayo ili kuwanusuru afya zao na magonjwa ya mlipuko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *