Shamba la Kilimanjaro Veggies lililopo wilayani Hai mkoani Kilimanjaro linalomilikiwa na Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe limesitishwa kufanyika shughuli za kilimo kutokana na kuwa ndani ya chanzo cha maji ya mto Weruweru.

Usitishwaji wa kilimo katika shamba hilo umetolewa na mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Gellasius Byakanwa baada ya kutembelea maeneo ya shamba hilo na kugundua uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji vya mto Weruweru.

Byakanwa amesema Mbunge huyo pia alifanya uharibifu wa mazingira kwa kuvuna miti ya asili bila kibali cha Mkuu wa Wilaya kulingana na maamuzi ya Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) pamoja na kuvuta maji kwa kutumia mashine kinyume na kibali na taratibu za utumiaji wa maji ya mfereji.

Mkuu wa Wilaya huyo amesema kuwa Mbowe ni kiongozi na ni kioo cha jamii hivyo haipendezi kufanya vitu kama hivyo kwani ni wajibu wa wananchi kuvitunza vyanzo hivyo na hakuna mradi utakaoruhusiwa kufanywa ndani ya mita 60 kutoka chanzo cha maji.

Pia mkuu wa wilaya amesema Januari 10, mwaka huu, alifanya ziara katika shamba hilo baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wananchi na mamlaka ya bonde la maji na kujionea hivyo alimwandika Mbowe barua ya wito wa kufika ofisi ya Mkuu wa Wilaya Januari 13, akiwa na vibali vinavyomruhusu kufanya shughuli za kibinadamu katika chanzo hicho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *