Wakuu wa Wilaya jijini Dar es Salaam na mkoa wa Pwani, wamelitaka Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) kuhakikisha kero sugu ya huduma ya maji katika Jiji la Dar es Salaam inaisha ifikapo mwaka 2020.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema wakati wa ziara ya wakuu wa wilaya za Dar es Salaam na Pwani katika mitambo ya uzalishaji maji iliyochini ya Dawasco.

Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa wilaya wenzake, Mjema alisema kuwa ziara hiyo imesaidia kuwapa mwanga wa shughuli zinazofanywa na Dawasco na hata kuona miradi mikubwa iliyofanywa na serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi na salama.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, aliyekuwapo katika ziara hiyo, Ally Happi alitoa mwito kwa Dawasco kuendelea kuunganishia wateja huduma ya maji kwa wakati na pia kupambana na wezi wa maji wanaokwamisha juhudi za mamlaka hiyo kwa kuiba maji na kuharibu miundombinu ya maji.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasco, Cyprian Luhemeja alieleza kuwa mamlaka hiyo inaendelea na kampeni ya kuwaunganisha wateja wapya na kueleza kuwa mpaka sasa muitikio wa sasa ni mkubwa tangu kuanza kwa kazi hiyo chini ya Kampeni ya Mama Tua Ndoo Kichwani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *