Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) imetangaza kuanzishwa kwa mfumo mpya wa ukataji wa tiketi za mabasi na daladala kwa njia ya kielektroniki.

Hatua hiyo ina lengo la kurahisisha upatikanaji wa mapato halali ya serikali pamoja na kuwafanya madereva na makondakta, kuajiriwa rasmi na wamiliki wa vyombo hivyo vya usafiri.

Pia mamlaka hiyo imezindua kampeni ya usafi kwa wafanyakazi wa daladala, ambayo inawataka kubadilisha sare za madereva na makondata, ambazo walishonewa na matajiri wao.

Sasa wafanyakazi hao watashona sare zao wao wenyewe ili wawe na uhalali wa kuzimiliki na kuzifanyia usafiri wa mara kwa mara.

Mkurugenzi wa Barabara wa Sumatra, Johansen Kahatano alisema jana kuwa mfumo huo wa tiketi za daladala kwa njia ya elektroniki, utaanza kutumika Januari mwaka kesho.

Ametangaza mfumo huo jana wakati wa uzinduzi wa kampeni ya usafi kwa madereva, ambayo inahusisha usafi wa mwili, mavazi na mabasi uliofanyika katika stendi ya Makumbusho, Dar es Salaam. Katika kampeni hiyo, madereva na makondakta watajishonea wenyewe sare zao na sio wamiliki wa magari.

Kahatano alisema chini ya mfumo wa ukataji wa tiketi kwa njia ya kielektroniki, utamfanya mmiliki wa basi kujua mapato yake halisi kwa siku na hivyo atawalipa wafanyakazi wake mshahara na Serikali itapata kiwango sahihi cha kodi. Kwa sasa ukataji wa tiketi za mabasi na ule wa daladala, unafanywa kwa tiketi zilizochapishwa.

Amesema kutokana na mfumo huo mpya, dereva haruhusiwi kumlipa mmiliki hesabu ya kila siku kama wanavyofanya sasa.

Badala yake, mmiliki ndiye atatakiwa kumlipa dereva na kondakta wa gari lake mshahara kila mwisho wa mwezi.

Amesema ili malipo hayo yaweze kufanyika ni lazima madereva waajiriwe rasmi na walipwe chini ya mfumo wa ajira.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *