Kamanda wa polisi Ilala, Salum Hamduni amewazuia wafuasi wa CUF wanaomuunga mkono Katibu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad kufanya usafi katika ofisi za chama hicho Buguruni siku ya Jumapili.

CUF walipanga kufanya usafi katika ofisi zao wakisema kuwa Profesa Lipumba amekuwa akitumia vibaya ofisi hiyo kwa kuifanya kijiwe cha wahuni kupanga mambo ya kihuni ikiwepo kupanga mipango ya kuvamia watu.

Wanachama wa CUF zaidi ya elfu tano na wabunge wa CUF 42 ambao wanamuunga mkono Maalim Seif wamepanga kwenda kusafisha ofisi ya chama chao CUF Makao Makuu Buguruni siku ya Jumapili ya tarehe 30 mwezi huu wa nne.

Mbunge wa Temeke kwa tiketi ya CUF, Abdallah Mtolea akiwa ameambatana na wabunge wengine 41 amesema wameamua kufanya usafi katika ofisi ya chama chao baada ya kuona ofisi hiyo imekuwa ikitumiwa vibaya Profesa Lipumba na genge lake kufanya mipango ya kuvamia mikutano ya watu, na matukio ya kihalifu.

Mbali na hilo Mtolea amesema wazo hilo lilianzia Temeke lakini limepokewa vyema na sehemu zingine hivyo baadhi ya wanachama kutoka Zanzibar, Tanga na wanachama wa maeneo jirani wataungana na wabunge 42 kufanya usafi huo hapo Buguruni.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *