Muimbaji mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Ally Choki amesema anatarajia kufanya tamasha kubwa la muziki kuadhimisha miaka 30 tangu kuanza kwake kuimba mwaka 1986.

Onesho hilo litakwenda sambamba na uzinduzi wa wimbo wake mpya unaofahamika kama Natamani na uzinduzi wa kitabu kinachoelezea historia ya maisha yake ya muziki.

Choki amesema tamasha hilo litafanyika Novemba 26, mwaka huu kwenye ukumbi wa Mango Garden na kushirikisha wasanii kadhaa wa zamani na sasa.

Choki amesema ataburudisha kwa nyimbo kumi, ikiwa ni mchanganyiko wa zamani na sasa ambazo zitakuwa ni kama zawadi kwa mashabiki watakaojitokeza siku hiyo.

Msanii huyo licha ya changamoto kadhaa alizopitia katika safari yake ya muziki amesema anajivunia kupata mafanikio mengi na zaidi akisisitiza umuhimu wa watu kushiriki naye siku hiyo na kujifunza mambo mengi aliyoyaandaa kupitia kitabu chake.

Choki amewahi kufanya kazi na bendi kibao za muziki nchini ikiwemo Kibaha Sound, Lola Afrika, Bantu Group, Twanga Pepeta na kuanzisha bendi yake ya Extra Bongo kabla ya kurudi tena Twanga.

Nyimbo alizowahi kuimba ni Baba Jeni, Gubu la Wifi, Chuki Binafsi, Jirani na nyingine kibao.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *