Mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa leo ataongoza mashambulizi katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya MC Alger ya Algeria Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kocha Mzambia, George Lwandamina tayari ametoa orodha ya wachezaji 11 wanoanza leo pamoja na sita watakaoanzia benchi.

Kikosi kimerudi karibu kile kile kilichoshinda 1-0 dhidi ya Azam katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara isipokuwa tu anakosekana kiungo Mzambia, Justin Zulu ambaye ni majeruhi.

Na badala yake leo ameendelea kucheza kiungo chipukizi, Said Juma ‘Makapu’ aliyempokea Jumamosi ya wiki iliyopita baada ya kuumia.

Lwandamina ametumia mfumo wa 4-3-3 akiwapanga Simon Msuva, Obrey Chirwa na Deus Kaseke kushambulia, wakati katika nafasi ya kiungo wapo Mnyarwanda Haruna Niyonzima, Thabani Kamusoko na Said Juma.

Langoni yupo kama kawaida ‘Yanga One’, Deogratius Munishi ‘Dida’, beki ya kulia Hassan Kessy, kushoto Mwinyi Hajji Mngwali na katikati Mtogo Vincent Bossou na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

Katika benchi wapo kipa Beno Kakolanya, mabeki Juma Abdul, Vincent Andrew ‘Dante’, viungo Emmanuel Martin, Geoffrey Mwashiuya na mshambuliaji Mzimbabwe Donald Ngoma.

Mchezo huo  utachezeshwa na marefa kutoka Rwanda, Louis Hakizimana atakayepuliza filimbi akisaidiwa na washika vibendera Theogene Ndagijimana na Jean Bosco Niyitegeka, wakati refa wa akiba atakuwa Ruzindana Nsoro na Kamisaa ni Ata Elmanan Hassan Osama kutoka Sudan.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *