Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli baada ya kuzuia usafirishaji wa mchanga wa dhahabu.

Chama hicho kimesema kuwa hakioni ulazima wa kusafirishwa mchanga huo nje ya nchi kwani inawezekana kujenga nchini mtambo wa kuchenjua makinikia ya mchanga huo.

Mara baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa watendaji wote wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Nchini (TMAA) na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kwa kile kilichodaiwa kushindwa kujenga kinu cha kuchenjulia makinikia tangu mwaka 2010, licha ya Sera ya Madini ya mwaka 2009 kuagiza.

Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe amesema suala la kujenga mtambo wa kuchenjua makinikia ya mchanga wenye madini ni muhimu kwa sasa na kwamba hilo linawezekana.

Ameongeza kuwa utafiti uliofanywa na ripoti yake kuwasilishwa katikati ya wiki na Kamati ya Profesa Abdulkarim Mruma si wa kwanza, kwani mambo yaliyoibuliwa yaliwahi kuibuliwa pia na Kamati ya Jaji Mark Bomani na pia mashirika ya nje, yote yakisisitiza kuwa mikataba ya madini nchini haiifaidishi nchi.

Pia asema hata wabunge wa kambi ya upinzani, kwa muda wamekuwa wakilalamikia mikataba iliyoingiwa baina ya Serikali na wawekezaji katika madini kuwa haikuwa na maslahi wala faida kwa watanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *