Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May ametia saini barua ambayo itaanzisha rasmi mchakato wa kuiondoa Uingereza kutoka kwa Muungano wa Ulaya.

Barua hiyo inatoa taarifa rasmi ya nchi ya Uingereza kujiondoa kwenye Umoja huo wa Ulaya kwa kutumia kifungu cha 50 cha mkataba wa Lisbon.

Barua hiyo itawasilishwa kwa rais wa Baraza la Ulaya, Donald Tusk baadaye leo kwaajili ya kutambua rasmi uamuzi huo.

Waziri huyo mkuu wa Uingereza, Theresa May baadaye hii leo anatarajiwa kulihutubia bunge la Uingereza na kuwaambia wabunge kwamba hatua hiyo inaashiria ‘wakati wa taifa la Uingereza kuungana pamoja’.

Brexit imekuja kufuatia kura ya maoni iliyoandaliwa mwezi Juni mwaka jana, ambapo wapiga kura wengi walipendekeza nchi hiyo kujiondoa kutoka kwenye EU.

Barua ya Bi May itawasilishwa kwa Bw Tusk leo na balozi wa Uingereza kwenye EU, Sir Tim Barrow.

Waziri mkuu ataongoza kikao cha baraza la mawaziri asubuhi, baadaye atatoa hotuba rasmi kwa wabunge kuthibitisha kwamba mchakato wa Uingereza kujiondoa EU umeanza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *