Bondia Mohamed Matumla Jr (30) ambaye alifanyiwa upasuaji wa kichwa hivi karibuni, ameruhusiwa jana kurudi nyumbani. Msemaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (MOI), Jezza Waziri alisema jana kuwa madaktari wamejiridhisha na afya ya bondia hiyo na kuamua kumruhusu huku wakifuatilia maendeleo yake kwa karibu.

“Afya ya Matumla imeimarika kwa kiasi kikubwa kwa sasa ataendelea kufuatiliwa kwa karibu kama wagonjwa wa nje kwenye kliniki yetu, hadi atakapopona kabisa,”alisema Waziri.

Matumla Jr alifanyiwa upasuaji wa kichwa hivi karibuni katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kulazwa katika wodi ya wagonjwa mahututi (ICU) kabla ya kuhamishiwa wodi ya kawaida baada ya siku chache.

Bondia huyo alipoteza fahamu akiwa ulingoni baada ya kupigwa ngumi na bondia Mfaume Mfaume na kudondokea kichwa katika raundi ya saba ya pambano la raundi 10 la uzani wa light na kushindwa kwa KO.

Bondia huyo baada ya kudondoka ulingoni hakuamka hadi alipofikishwa Hospitali ya Wilaya Temeke, alipatiwa huduma na kuzinduka kabla ya kuhamishiwa Moi ambako alilazimika kufanyiwa upasuaji wa kichwa.

Source: Habari Leo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *