Nahodha wa Klabu ya Azam FC John Bocco amesema anaamini kikosi hicho kitakuwa vizuri na kukaa nafasi nzuri kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara.
Bocco amesema morali waliyokuwa nayo wachezaji pamoja na nguvu za nyota wapya walioongezwa kikosini kwenye usajili huu wa dirisha dogo, utaweza kuwasaidia kufanya vizuri.
Benchi la Ufundi la Azam FC kwa kushirikiana na uongozi wa timu hiyo, katika usajili huu wa dirisha dogo unaoendelea umeweza kuongeza nguvu mpya kwa kuwasajili washambuliaji nyota wawili kutoka Ghana, Yahaya Mohamed anayetokea Aduana Stars na staa wa Sekondi Hasaacas na Samuel Afful
Pia imewarudisha kundini wachezaji wake wawili waliokuwa kwa mkopo, beki wa kati kinda Abdallah Kheri aliyekuwa Ndanda na winga wa kushoto Enock Atta Agyei (Medeama).
Azam FC mpaka inamaliza mzunguko wa kwanza wa ligi imefanikiwa kujikusanyia jumla ya pointi 25 katika nafasi ya tatu kwenye msimamo ikizidiwa pointi 10 na kinara Simba aliyejikusanyia pointi 35 na Yanga ikiwa na pointi 33.