Serikali imesema imetenga Sh bilioni 70 kwa ajili ya kukabili ukosefu wa dawa nchini, huku ikitangaza kujenga kiwanda cha dawa mkoani Simiyu.

Hayo yamesemwa na makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Wataalamu wa Sekta ya Afya, wakiwamo waganga wa mikoa na wilaya.

Awali akimkaribisha Makamu wa Rais, Mwenyekiti wa Waganga hao, Dk Sudi Leonard katika risala, alisema kuna tatizo la ukosefu wa dawa na vifaa tiba katika baadhi ya vituo vya afya nchini hali ambayo inazua malalamiko kwa wananchi.

Pamoja na utoaji wa fedha kwa ajili ya kuondoa tatizo hilo, Makamu wa Rais alisema mpango wa muda mrefu wa serikali ni kuwa na kiwanda cha dawa na kwamba mpango upo wa kujenga kiwanda hicho katika mkoa wa Simiyu.

Vilevile aliitaka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kuhakikisha waganga wa tiba asili wote wanasajiliwa kutokana na umuhimu wao katika jamii. “

Tiba mbadala na tiba asili ni taaluma yenye asili ya Kiafrika tuliyorithi kutoka kwa mababu zetu kutokana na uhitaji wake mkubwa ninaagiza wizara kuhakikisha waganga wa tiba asili wote wanasajiliwa na wanafahamika,” alisema. Aliwataka wataalamu hao wa afya, kutosita kuwachukulia hatua kali za kinidhamu wote wanaobainika kukiuka maadili na viapo vyao vya kazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *