Biashara zimefungwa mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Kinshasa na hakuna magari barabarani kufuatia wito wa upinzani kwa watu wakae ndani ili kushinikiza uchaguzi mkuu nchini ufanyike Novemba na Rais Kabila ajiuzulu.

Taarifa zinasema vikosi vya usalama vimeizingira nyumba ya mpinzani mkuu wa rais Kabila, Etienne Tshisekedi, ambye ndiye anayongoza wito wa uchaguzi ufanyike Novemba mwaka huu.

Chama chake kimeonya kuwa rais Kabila atakuwa anatekeleza uhaini wa hali ya juu iwapo uchaguzi utacheleweshwa.

Katiba inamzuia Kabila kuwania muhula wa tatu, na upinzani unatuhumu kuwa serikali inataka kuchelewesha uhaguzi huo ili Kabila asalie madarakani.

Chama tawala na kimoja cha upinzani vimependekeza kuchelewesha uchaguzi wa urais hadi Aprili 2018.

Tume ya uchaguzi imesema inahitaji muda zaidi kuweka sawa orodha ya wapiga kura.

Watu kadhaa wameuawa Kinshasa mwezi uliopita katika maandamano ya kumtaka rais Kabila aondoke madarakani Desemba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *