Klabu ya soka ya Barcelona imesema haitasafiri na mashabiki wake kwenye mchezo wa La Liga dhidi ya Atletico Madrid wiki ijayo kwenye uwanja wa Wanda Metropolitano jijini Madrid.

Uongozi wa Barcelona umetuma taarifa kwa viongozi wa Atletico Madrid ukiwataka wasiuze tiketi kwaajili ya mashabiki wa timu hiyo bali wauze tiketi kwa mashabiki wa Atletico pekee.

Barcelona imefikia uamuzi huo kufuatia vuguvugu lililopo nchini Hispania ambapo Wananchi wa Jimbo la Catalonia yalipo makao makuu ya klabu hiyo wamepiga kura ya kujitenga kutoka nchi ya Hispania.

Mechi iliyopita ya Barcelona dhidi ya Las Palmas kwenye uwanja wa Camp Nou timu hizo pia zilicheza bila mashabiki sababu kubwa ikiwa ni hofu ya mashaabiki kufanya vurugu na kupelekea umwagaji damu.

Hatua ya Barcelona kugoma kusafiri na mashabiki ni mwendelezo wa hofu ya kutokea vurugu kutokana na uhasama unaoonekana kati ya Wananchi wa jiji la Madrid ambao wanaunga mkono serikali ya Hispania na wale wa Barcelona ambao wanaunga mkono serikali ya Catalonia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *