Balozi wa Kenya nchini Tanzania Chirau Ali Mwakwere amejiuzulu nafasi hiyo ili apate nafasi ya kuwania uongozi kwenye uchaguzi mkuu nchini Kenya mwaka huu.

Mwakwere, ambaye amekuwa balozi wa Kenya tangu mwanzoni mwa mwaka 2015, amejiuzulu rasmi Ijumaa kumuwezesha kuwania nafasi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti mwaka huu.

Balozi huyo ambaye mwishoni mwa wiki alitangaza rasmi kuhamia chama cha upinzani cha ODM, alikuwa awali mwanachama wa chama cha URP, moja ya vyama vilivyounda muungano wa Jubilee ulioshinda uchaguzi mkuu mwaka 2013.

Aliwania wadhifa wa seneta katika uchaguzi huo lakini akashindwa na Boy Juma Boy wa chama cha ODM.

Mwakwere ni miongoni mwa waliotangaza nia ya kuwania wadhifa wa ugavana katika kaunti ya Kwale, baada ya gavana wa sasa Salim Mvurya kuhama chama cha ODM na kujiunga na chama Jubilee chake Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto.

Mwakwere, 71, alihudumu kama waziri wa mambo ya nje wa Kenya kati ya 2004 na 2005 na baadaye akateuliwa waziri wa uchukuzi Desemba 2005.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *