Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amesema kuwa baadhi ya wizara  zitatumia majengo ya chuo cha Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Mhagama amesema hayo wakati akitoa ufafanuzi kuhusu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Lyimo (Chadema) aliyeshangaa wizara kutumia majengo ya Udom, akadai ni kuchanganya wizara na elimu.

Lyimo aliuliza swali la nyongeza kutokana na swali la msingi, lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Jasmine Bunga (CCM) aliyehoji lini serikali itaanza kujenga miundombinu mipya ya Chuo Kikuu Mzumbe, akahoji kwa nini wizara imehamia Dodoma na kutumia majengo ya Udom, haioni kwamba ni kuchanganya elimu na wizara.

Waziri Jenista alifafanua akisema, mpango wa kuhamia Dodoma na kutumia majengo ya Udom, ni utaratibu wa kawaida wala hauna lengo la kuvuruga masomo au kuingiliana na wizara na taaluma chuoni hapo, isipokuwa ni kutokana na Udom kuwa na majengo mengi ambayo yalikuwa hayatumiki.

Alisema, Udom ilianzishwa kutokana na nia ya CCM kwa lengo la kupanua elimu kuwafikia Watanzania wengi, lakini majengo mengi yamebaki bila kutumika hivyo, wizara kuyatumia katika kipindi hiki si vibaya.

Awali, akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Stella Manyanya alisema kitendo cha wizara kutumia majengo ya Udom ni kitendo cha muda mfupi, wakati serikali ikijipanga ili kila wizara kuwa na majengo yake.

Alisema Mamlaka ya Ustawishaji Makao Mkuu (CDA), itajenga majengo kwa ajili ya wizara, hivyo kwa sasa majengo ya Udom yanaweza kutumika na wizara.

Wakati huo huo, kutokana na kutoridhishwa na majibu ya waziri Jenista, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), ameendeleza hoja ya kupinga hatua ya serikali kuhamishia baadhi ya wizara (Udom).

Katika mwongozo wake alioutoa kwa kiti cha Spika mjini Dodoma jana, mbunge huyo aliitaka serikali itoe ufafanuzi juu ya taratibu za kielimu ili kubaini kama zinaruhusu wanafunzi wa elimu ya juu kuchanganywa na watu wengine katika maeneo ya kujifunzia.

Source: Habali Leo

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *