Baada ya uteuzi wake kutenguliwa na Rais Magufuli, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini na Mbunge wa Musoma Vijiji Prof. Sospeter Muhongo amewasihi wakazi wa jimbo hilo kutokuingiwa na hofu kufuatia uamuzi kutimuliwa uwaziri.
Prof. Muhongo amewataka wananchi wa jimbo hilo na rafiki zake kutokuwa na hofu kwani kwa pamoja watafanikiwa.
Kwa mujibu wa taarifa za ofisi yake, amewaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha kuwa wanafikia malengo yao ya kimaendeleo kwa kutimiza ahadi zake.
Taarifa hiyo ilitolewa na Katibu wa Mbunge huyo, Juma Ramadhan ambaye amesema kuwa kilichotokea ni cha kawaida kwenye siasa na inawapasa kusahau hayo ili waweze kusonga mbele katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Wakazi wa jimbo hilo waliahidi kutoa ushirikiano kwa mbunge wao katika kutekeleza miradi hiyo kwani yeye si kiongozi wa kwanza kuondolewa kwenye wadhifa wake. Aidha, wakazi hao walisema kuwa kuondolewa kwa Prof. Muhongo kuwe funzo kwa wateule wengine kuwa nafasi hizo si za kudumu.
Mbunge huyo wa Musoma vijijni Muhongo alifutwa kazi kufuatia kushindwa kusimamia kwa umakini sekta ya madini na hivyo kupelekea serikali kupata hasara.