Kesi inayowakabili viongozi wa Simba, Evans Aveva na Geofrey Nyange ‘Kaburu’ imeendelea leo katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
Upande wa mashitaka katika kesi hiyo umesema kuwa wanaendelea na uchunguzi na kwamba wamepeleka nyaraka kwa mtaalamu wa maandishi hivyo wanasubiri ripoti .
Wakili wa Serikali, Esterzia Wilson amedai leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa shauri hilo limekuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi bado haujakamilika.
Wakili wa washitakiwa, Evodius Mtawala amedai mahakama ilipanga tarehe ya jana kwa ajili ya kusisitiza upande wa mashitaka kuharakisha upelelezi hivyo wanaomba tarehe ya karibu. Hakimu Nongwa aliutaka upande wa mashitaka kujitahidi kupata ripoti hiyo kwa kuwa washitakiwa wako gerezani na kwamba wangekuwa nje wasingesumbuliwa sana.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka ya kughushi na kutakatisha fedha. Inadaiwa Machi 15, mwaka jana, jijini Dar es Salaam, washitakiwa wote kwa pamoja walighushi fomu ya kuhamisha fedha kuonesha kwamba Klabu ya Simba inalipa deni la Dola za Marekani 300,000 kwa Aveva, kitu ambacho si kweli.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 8 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa tena mahakamani hapo kwa ajili ya kusikilizwa.